8
Kuwekwa Kwa Taa
Bwana akamwambia Mose, “Sema na Aroni umwambie, ‘Wakati utakapoziweka zile taa saba, zinatakiwa kuangaza eneo lililo mbele ya kinara cha taa.’ ”
Aroni akafanya hivyo; akaziweka zile taa ili zielekee mbele kwenye kinara cha taa, kama vile Bwana alivyomwamuru Mose. Hivi ndivyo kinara cha taa kilivyotengenezwa: Kilitengenezwa kwa dhahabu iliyofuliwa, kuanzia kwenye kitako chake hadi kwenye maua yake. Kinara cha taa kilitengenezwa sawasawa kabisa na kielelezo ambacho Bwana alikuwa amemwonyesha Mose.
Kutengwa Kwa Walawi Kwa Ajili Ya Bwana
Bwana akamwambia Mose: “Watwae Walawi kutoka miongoni mwa Waisraeli wengine na uwatakase kwa kawaida ya ibada. Ili kuwatakasa fanya hivi: Nyunyizia maji ya utakaso juu yao; kisha uwaambie wanyoe nywele kwenye mwili mzima, wafue nguo zao na hivyo wajitakase wenyewe. Waambie wamchukue fahali mchanga pamoja na sadaka yake ya nafaka ya unga laini uliochanganywa na mafuta; kisha utamchukua fahali mchanga wa pili kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Walete Walawi mbele ya Hema la Kukutania na ukusanye jumuiya yote ya Waisraeli. 10 Utawaleta Walawi mbele za Bwana, na Waisraeli wataweka mikono yao juu ya Walawi. 11 Aroni atawaweka Walawi mbele za Bwana kama sadaka ya kuinua kutoka kwa Waisraeli, ili kwamba wawe tayari kuifanya kazi ya Bwana.
12 “Baada ya Walawi kuweka mikono yao juu ya vichwa vya hao mafahali wawili, tumia mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi kwa Bwana, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Walawi. 13 Waambie hao Walawi wasimame mbele ya Aroni na wanawe, kisha wawatoe kama sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana. 14 Kwa njia hii utakuwa umewatenga Walawi kutoka kwa Waisraeli wengine, nao Walawi watakuwa wangu.
15 “Utakapokuwa umekwisha kuwatakasa Walawi na kuwatoa kama sadaka ya kuinuliwa, watakuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania. 16 Wao ndio Waisraeli ambao watatolewa kabisa kwangu. Nimewatwaa kama mali yangu mwenyewe badala ya mzaliwa wa kwanza, mzaliwa wa kwanza wa kiume kutoka kwa kila mwanamke wa Kiisraeli. 17 Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume katika Israeli, awe wa mwanadamu au mnyama, ni wangu. Wakati nilipowaua wazaliwa wote wa kwanza huko Misri, niliwatenga kwa ajili yangu mwenyewe. 18 Nami nimewatwaa Walawi badala ya wazaliwa wote wa kwanza wa kiume katika Israeli. 19 Kati ya Waisraeli wote, nimempa Aroni na wanawe Walawi kama zawadi ili wafanye kazi katika Hema la Kukutania kwa niaba ya Waisraeli, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili pasiwepo na pigo lolote litakalowapata Waisraeli wakati watakapokaribia mahali patakatifu.”
20 Mose, Aroni na jumuiya yote ya Waisraeli wakawafanyia Walawi kama Bwana alivyomwamuru Mose. 21 Walawi wakajitakasa wenyewe na wakafua nguo zao. Kisha Aroni akawasogeza mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili kuwatakasa. 22 Baada ya hayo, Walawi walikuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania chini ya usimamizi wa Aroni na wanawe. Waliwafanyia Walawi kama vile Bwana alivyomwamuru Mose.
23  Bwana akamwambia Mose, 24 “Hili linawahusu Walawi: Wanaume wenye umri wa miaka ishirini na mitano au zaidi watakuja kushiriki katika kazi kwenye Hema la Kukutania, 25 lakini watakapofika umri wa miaka hamsini, ni lazima waache kazi zao za kawaida wala wasiendelee. 26 Wanaweza kuwasaidia ndugu zao kufanya wajibu wao katika Hema la Kukutania, lakini wao wenyewe kamwe hawatafanya hiyo kazi. Basi, hivi ndivyo utakavyogawa wajibu kwa Walawi.”