53
Ni nani aliyeamini ujumbe wetu,
na mkono wa Bwana umefunuliwa kwa nani?
Alikua mbele yake kama mche mwororo
na kama mzizi katika nchi kavu.
Hakuwa na uzuri wala utukufu wa kutuvutia kwake,
hakuwa na chochote katika sura yake cha kutufanya tumtamani.
Alidharauliwa na kukataliwa na wanadamu,
mtu wa huzuni nyingi, ajuaye mateso.
Kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,
alidharauliwa, wala hatukumhesabu kuwa kitu.
 
Hakika alichukua udhaifu wetu
na akajitwika huzuni zetu,
hata hivyo tulidhania kuwa amepigwa na Mungu,
akapigwa sana naye, na kuteswa.
Lakini alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu,
alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu;
adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake,
na kwa majeraha yake sisi tumepona.
Sisi sote, kama kondoo, tumepotea,
kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe,
naye Bwana aliweka juu yake
maovu yetu sisi sote.
 
Alionewa na kuteswa,
hata hivyo hakufungua kinywa chake;
aliongozwa kama mwana-kondoo
apelekwaye machinjoni,
kama vile kondoo anyamazavyo mbele ya wao wamkataye manyoya,
hivyo hakufungua kinywa chake.
Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa.
Nani awezaye kueleza kuhusu kizazi chake?
Kwa maana alikatiliwa mbali na nchi ya walio hai,
alipigwa kwa ajili ya makosa ya watu wangu.
Wakamfanyia kaburi pamoja na waovu,
pamoja na matajiri katika kifo chake,
ingawa hakutenda jeuri,
wala hapakuwa na hila kinywani mwake.
 
10 Lakini yalikuwa ni mapenzi ya Bwana
kumchubua na kumsababisha ateseke.
Ingawa Bwana amefanya maisha yake
kuwa sadaka ya hatia,
ataona uzao wake na kuishi siku nyingi,
nayo mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake.
11 Baada ya maumivu ya nafsi yake,
ataona nuru ya uzima na kuridhika;
kwa maarifa yake, mtumishi wangu mwenye haki
atawafanya wengi kuwa wenye haki,
naye atayachukua maovu yao.
12 Kwa hiyo nitamgawia sehemu miongoni mwa wakuu,
naye atagawana nyara pamoja na wenye nguvu,
kwa sababu aliyamimina maisha yake hadi mauti,
naye alihesabiwa pamoja na wakosaji.
Kwa kuwa alichukua dhambi za wengi,
na kuwaombea wakosaji.